Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) kimshiriki Mkutano Mkuu wa Sita wa Shirikisho la Kimataifa la Wafanyakazi wa Ujenzi na Mbao (BWI), uliofanyika tarehe 16-20 Novemba 2026 jijini Sao Paulo, Brazil.
Mkutano huo, uliofanyika chini ya kaulimbiu “NO STEP BACK! Together, Stronger, Forward”, uliwakutanisha wajumbe 548 kutoka vyama 237 vya wafanyakazi katika nchi 69 kujadili mustakabali wa harakati za wafanyakazi, kupitisha maazimio, kuchagua viongozi na kuweka mwelekeo wa kimkakati wa shirikisho kwa miaka ijayo.
Ujumbe wa TUICO uliongozwa na Katibu Mkuu, Ndg. CPA Silvester Issaya Mrope, ukiwahusisha Mkuu wa Sekta ya Fedha, Ndg. Lisungu Mapunda, Mkuu wa Idara ya Fedha na Utawala, CPA Beatrice Ouko, pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mahusiano, Ndg. Venance Majula.
Akizungumzia umuhimu wa ushiriki wa TUICO katika mkutano huo, Katibu Mkuu alisema:
“Mitaji inavuka mipaka ya nchi, na mshikamano wa wafanyakazi lazima uvuke mipaka hiyo pia. Tunarejea na maarifa na uzoefu utakaotusaidia kuimarisha TUICO na kuleta matokeo yenye manufaa kwa wanachama wetu.”
Kuimarisha uwakilishi na nguvu ya wafanyakazi
Kupitia mikutano na mijadala mbalimbali, TUICO ilibadilishana uzoefu na vyama vya wafanyakazi kutoka sehemu mbalimbali duniani kuhusu mikakati ya uhamasishaji, majadiliano ya pamoja, afya na usalama kazini, uwajibikaji wa kampuni za kimataifa na ulinzi wa haki za wafanyakazi katika mazingira ya mabadiliko ya teknolojia na tabianchi.
Mijadala hiyo ina umuhimu wa moja kwa moja kwa wanachama wa TUICO katika viwanda vya saruji na vifaa vingine vya ujenzi, hususan katika kuimarisha matawi, kuboresha mishahara na mazingira ya kazi, kulinda usalama wa ajira na kuongeza nguvu ya wafanyakazi katika majadiliano na waajiri.
Katika mjadala kuhusu nafasi ya wafanyakazi katika mnyororo wa uzalishaji wa vifaa vya ujenzi na maendeleo ya miundombinu, TUICO ilishirikisha uzoefu wake katika kuhamasisha wafanyakazi, kuanzisha na kuimarisha matawi, kufanya majadiliano ya pamoja na kutetea haki za wafanyakazi katika kampuni za ndani na za kimataifa.
Vijana, uchumi usio rasmi na uimarishaji wa vyama
Miongoni mwa masuala yaliyopewa umuhimu katika mijadala ni namna ya kujenga vyama vya wafanyakazi vinavyokidhi mahitaji ya kizazi kipya na wafanyakazi walio katika uchumi usio rasmi.
Uzoefu uliowasilishwa na vyama mbalimbali ulionesha umuhimu wa kuunganisha uhamasishaji na huduma zinazoboresha maisha ya wafanyakazi, ikiwemo elimu, ukuzaji wa ujuzi, mafunzo kwa vitendo, hifadhi ya jamii na utetezi wa haki zao.
Kwa TUICO, maarifa hayo yanatoa fursa ya kuimarisha mikakati ya kuongeza na kudumisha wanachama, kupanua uwakilishi katika uchumi usio rasmi na kukuza ushiriki wa vijana.
Kuimarisha mahusiano ya kimataifa
Katika kutambua na kuthamini ushirikiano uliopo kati ya TUICO na BWI, Katibu Mkuu wa TUICO alikabidhi tuzo ya shukrani kwa Katibu Mkuu mpya wa BWI, Bi. Paola Cammilli.
Ujumbe wa TUICO pia uliwasilisha zawadi za kumbukumbu kwa Katibu Mkuu aliyemaliza muda wake wa uongozi wa BWI, Ndg. Ambet Yuson, Makamu wa Rais mpya wa BWI kutoka Chama cha Kitaifa cha Wafanyakazi wa Migodini cha Afrika Kusini (NUM) Ndg. Manzaba Phillip Vilakazi, pamoja na Katibu Mkuu wa IndustriALL Global Union, Ndg. Atle Høie.
Shughuli hizo zilikuwa sehemu ya jitihada za TUICO za kuimarisha mahusiano ya kitaasisi na kupanua fursa za ushirikiano katika uhamasishaji, elimu na mafunzo, majadiliano ya pamoja na utetezi wa haki za wafanyakazi.
Hatua inayofuata
Kufuatia kuhitimishwa kwa mkutano huo, kipaumbele cha TUICO ni kuoanisha maazimio na mwelekeo mpya wa kimkakati wa BWI na Mpango Mkakati wa Saba wa TUICO wa mwaka 2026-2030.
Hatua hiyo inalenga kutumia maarifa, uzoefu na fursa za ushirikiano zilizopatikana kuimarisha utekelezaji wa vipaumbele vya Chama, hususan kuongeza wanachama, kuboresha huduma, kuimarisha majadiliano ya pamoja, kukuza uongozi wa vijana na kujenga uwezo wa viongozi na watendaji wa Chama.